Jumanne 26 Mei 2026 - 21:03
Wamarekani wajue kwamba muda haurudi nyuma/ Kujitenga na washirikina kwa hakika; ni jambo linalozidi msimu wa Hija

Hawza/ Ayatullah Sayyid Mujtaba Husseini Khamenei, Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, katika ujumbe wake kutokana na mnasaba wa kuwadia kwa msimu wa Hija ya Ibrahim, amezitaja ibada na adhkari zenye siri nyingi za Hija kuwa ni alama za kudumu kwa wanadamu wote katika kuhama kumuelekea Mwenyezi Mungu Mtukufu, kujikomboa kutoka katika vifungo vya Shetani na wafuasi wake, kufanya juhudi zisizokatika za kutekeleza majukumu ya Mwenyezi Mungu, kujinasua kutoka katika matamanio ya nafsi, na kupata fanaka ya duniani na Akhera.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, maandishi ya ujumbe wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa Umma wa Kiislamu, ambao ulisomwa asubuhi ya leo katika Jangwa la Arafat na Hujjatul-Islam wal-Muslimin Nawwab, mwakilishi wa Walii Faqih na mkuu wa mahujaji wa Iran, ni kama ifuatavyo:

Bismillahir-Rahmanir-Rahim

Labbaika Allahumma Labbaik, Labbaika La Sharika Laka Labbaik, Innal Hamda wan-Ni‘mata Laka wal-Mulk

Ewe Mola! Nimeitikia mwito Wako. Huna mshirika. Sifa zote, neema zote, ufalme wote na mamlaka yote vinatoka Kwako na ni Vyako.

Msimu wa Hija wa mwaka huu pia umefika, na mahujaji wa Umma wa Kiislamu wamevaa ihramu ya utiifu na kutamka Talbiya ili wahame kutoka maisha ya kimada na ya kawaida kwenda kwenye maisha ya kimungu na yenye fanaka; maisha ya Tauhidi yanayozunguka utiifu kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu Jal-la wa ‘Ala, pamoja na kukataa, kuondoa na kujitenga na wanaomshikisha wa Mwenyezi Mungu. Lakini fursa ya hijra hii si ya wageni na mahujaji wa mwaka huu wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu pekee; bali inawahusu ndugu na dada wote Waislamu wa Iran na ulimwenguni kote, kuanzia wale waliokwisha kuwa mahujaji katika miaka iliyopita ya maisha yao hadi wale ambao bado hawajafanikiwa kutekeleza ibada za Hija.

Sharti la hijra hii ni kufunga ihramu ya kudumu inayozunguka dhikri ya Mwenyezi Mungu; ni kutufu daima kuzunguka mhimili wa haki; ni kufanya sa‘yi ya kudumu katikati ya vilele muhimu vya majukumu ya Mwenyezi Mungu; ni kumpiga mawe daima Shetani mwovu pamoja na sura zake zote za udanganyifu na wafuasi wake wote; ni kusimama kwa mazingatio na unyenyekevu; ni kumlisha masikini asiyeweza kujikimu na msafiri; ni kuchinja matamanio na mielekeo potofu, na kuondoa uchafu wa ndani; na katika hali zote kuwa tayari kufanya khidma na kuinua bendera ya kuitetea haki.

Na hivi ndivyo ilivyokuwa kwamba taifa la Iran katika miqat ya Mapinduzi ya Kiislamu liliingia katika njia ya hijra hii; likaitikia wito wa Kiibrahimu wa Imam Khomeini Mkuu; likavua vazi la kukubali utawala wa wengine; likavaa ihramu ya fanaka ya duniani na Akhera; na kwa kutamka Labbaik na kwa juhudi kubwa likajitahidi kutufu kuzunguka maarifa ya Uislamu safi wa Muhammad (saww) na kujikuribisha kwenye nuru inayong’ara ya uadilifu wa ulimwengu wote na Wilayah Kuu.

Allahu Akbar, Allahu Akbar, La ilaha illa Allah, Wallahu Akbar; Allahu Akbar wa Lillahil Hamd; Allahu Akbar ‘ala ma Hadana.

Ndiyo, Allahu Akbar! Na kwa silaha hii ya Allahu Akbar ndipo taifa la Kiislamu la Iran liliposimama miaka 47 iliyopita, likaangusha utawala wa kitwaghuti, kidikteta na tegemezi wa Pahlavi, likakata mikono na miguu ya Marekani mwenye tamaa na kiburi kutoka nchini, na likakatiza kabisa ushawishi wa Uzayuni.

Kwa silaha hii ya Allahu Akbar pia, baada ya uvamizi wa utawala wa Baath wa Saddam dhidi ya ardhi ya Iran, wapiganaji mashujaa na vijana waliojitoa muhanga waliandika Ulinzi Mtakatifu, na licha ya uungwaji mkono wa madola yote ya Mashariki na Magharibi kwa utawala wa Baath, waliuweka mahali pake. Na waliendeleza msimamo huu kwa uthabiti kwa miaka mingi baadaye mbele ya mzingiro wa kiuchumi, mapinduzi ya kijeshi, vikwazo vya kidhalimu na mashambulizi mengi ya kisiasa, kipropaganda na kiuchumi ya maadui dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Allahu Akbar! Ni silaha hii ya Allahu Akbar iliyozifanya imara nyuzi za muungano wa Umma wa Kiislamu na vijana wapiganaji wa Muqawama kutoka Iran hadi Lebanon, Palestina, Iraq na Syria; kutoka Afrika na Yemen hadi Afghanistan, Pakistan na mataifa yote huru duniani; ili kamba hii madhubuti isimame kutetea uwepo wa Umma wa Kiislamu mbele ya wavamizi waporaji wa Kizayuni, imvuruge kabisa Daesh, ianzishe Tufani al-Aqsa na kuufikisha utawala dhaifu wa Kizayuni kwenye hatua ya kuhesabu pumzi zake za mwisho.

Allahu Akbar! Ndiyo, Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mkuu zaidi kuliko anavyoweza kuelezwa, ilikuwa ni kwa silaha hii ya Allahu Akbar Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa kutegemea silaha hiyo, iliweza kuufanya utawala wa Kizayuni ushindwe katika vita vya pili vya kulazimishwa mnamo Khordad 1404, kuipiga kofi kali Marekani mvamizi na kumfanya adui ashindwe katika lengo lake la kuisalimisha Iran.

Na silaha ya Allahu Akbar ililipa taifa la Iran nguvu na uwezo mkubwa kiasi kwamba baada ya tukio lenye majonzi la kuuawa shahidi kwa Kiongozi Mkuu mtukufu, mrithi mwema wa Mtume Mtukufu (saww), Ayatullah al-Udhma Sayyid Ali Husseini Khamenei, [A‘la Allahu Maqamahu ash-Sharif], kwa mikono ya waovu wa dunia ya leo, taifa hili lilipata mwamko wa kimungu na kwa uwepo wake wa pande zote katika kila uwanja uliohitajika, likayafanya macho ya dunia yatizame mafanikio yake.

Kwa hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mkuu zaidi kuliko anavyoweza kuelezwa, kwa silaha hii ya Allahu Akbar wapiganaji mashujaa na vikosi vya jeshi vilivyojitolea mhanga ndani ya Iran, kwa kushirikiana na wapiganaji wa Muqawama hususan Lebanon mpendwa, walipata ushindi mkubwa dhidi ya majeshi mawili ya kigaidi ya Marekani na Wazayuni yaliyokuwa yamejihami hadi meno katika vita vya tatu vya kulazimishwa. Kwa kumtegemea Mola wao, walimrushia mawe Shetani Mkubwa yaani Marekani na mnyama aliyefundishwa na kulelewa naye, yaani utawala wa Kizayuni, kwa kutumia makombora na ndege zisizo na rubani ardhini, angani na baharini; na wakaiona kwa macho yao ahadi ya kweli ya Mwenyezi Mungu ya kuwapa nusura wanaopigana katika njia Yake.

Na tena Allahu Akbar! Bila shaka Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mkuu zaidi kuliko anavyoweza kuelezwa, na majeshi Yake yanashinda kila nguvu, na kwa silaha hii ya Allahu Akbar, baada ya mwamko wa taifa la Iran na Jabhat al-Muqawama, mwamko wa Umma wa Kiislamu utatokea, na kujitenga na washirikina kutasambaa kutoka tendo la kurusha mawe kwenye Jamarat za Hija hadi katika nyanja za maisha binafsi, kijamii na kisiasa ya Waislamu katika pembe zote za dunia, Umma wa Kiislamu na mataifa ya eneo hili vina uwezo mwingi na maslahi ya pamoja ambayo yataunda mfumo mpya na jiometri ya baadaye ya eneo hili na dunia.

Mimi kwa ukweli na ikhlasi ninazialika nchi zote na serikali zote za Kiislamu kwenye urafiki na kushirikiana katika mema na wema, ili kwa ushirikiano wao wachukue hatua katika njia ya maendeleo ya Umma wa Kiislamu na kutatua matatizo ya ulimwengu wa Uislamu.

Jambo lililo wazi katika suala hili ni kwamba; mshale wa wakati haurudi nyuma, na mataifa pamoja na ardhi za eneo hili havitakuwa tena ngao za kulinda kambi za Marekani, Marekani mbali na kwamba haitakuwa tena mahali salama kwa uovu na uwekaji wa vituo vya kijeshi katika eneo hili, kila siku inazidi kuachana na hali yake ya zamani, aidha utawala dhaifu na uvimbe wa saratani wa Kizayuni nao umeikaribia hatua ya mwisho ya maisha yake mabaya, na kwa fadhila za Mwenyezi Mungu, kwa mujibu wa kauli thabiti na yenye mtazamo wa mbali ya miaka 10 aliyopita ya Kiongozi Mkuu shahidi, Qaddasallahu Nafsahu az-Zakiyyah, hautaiona miaka 25 baada ya tarehe hiyo, Inshaallah.

Kwa sababu hiyo, mwaka huu suala la kujitenga na washirikina lina umuhimu maradufu, na kina pamoja na upana wa kujitenga na Marekani na utawala wa Kizayuni vinapita mipaka ya ibada ya kujitenga katika msimu na miqat ya Hija.

Katika maeneo mbalimbali ya Iran na duniani, baada ya siku hizi tukufu, kauli mbiu ya “Mauti kwa Marekani” na “Mauti kwa Israel” itakuwa kauli mbiu ya kawaida ya Umma wa Kiislamu na watu waliodhulumiwa duniani, hususan vijana.

Mustakabali ni wa Umma wa Kiislamu na ustaarabu mpya wa Kiislamu, na kila mmoja wetu anaweza, kwa kadiri ya hima yake, uwezo wake na wajibu wake, kutekeleza jukumu katika kufanikisha mustakabali huo na kuusogeza karibu zaidi, wageni na mahujaji wa Iran katika Hija ya mwaka huu wana jukumu muhimu na lenye kuonekana katika kusimulia ushindi wa vita vya tatu vya kulazimishwa kwa ndugu na dada zao Waislamu wengine na kuwapa matumaini kuhusu mustakabali mwema.

Ninawaomba mahujaji wote wapendwa maombi yao yawe kwa ajili ya kuharakishwa kudhihiri kwa Mwokozi wa wanadamu, Imam wa Zama (Ajjalallahu Ta‘ala Farajah), na wauombee umoja wa Umma wa Kiislamu, ukombozi wa Palestina na Msikiti wa al-Aqsa, kuondolewa kwa matatizo makubwa ya Waislamu na kufikiwa kwa ushindi wa mwisho dhidi ya ubeberu wa dunia, pia wanijumuishe mimi katika dua zao njema.

Ewe Mola! Teremsha rehema na baraka za Muhammad na Aali wa Muhammad, (saww) Uwajalie mahujaji na Umma wote wa Kiislamu mtazamo wa fadhila na huruma Yako, wajaalie Hija iliyokubaliwa, ziangazie nyoyo zao kwa nuru za maarifa na utambuzi, imarisha azma na irada yao katika njia ya kurekebisha hali ya Umma na kupata ushindi wa mwisho dhidi ya maadui wa Uislamu.

Ewe Mola! Teremsha fadhila na rehema Zako pana juu ya roho takatifu za mashahidi wa njia ya Mwenyezi Mungu, hususan mashahidi wa Jabhat al-Muqawama, na juu ya wote waliokuwa chini ya uongozi wao, na mbele yao Kiongozi Mkuu shahidi, "A‘la Allahu Maqamahu ash-Sharif", wafikishie thawabu nyingi za Hija ya mahujaji, ibada za wanaoabudu na juhudi za wale waliokuwa chini ya mwongozo wa Kiongozi wa Umma kwa roho yake ya kimalaika, ulisaidie taifa la Iran na Umma wa Kiislamu katika kuendeleza njia na malengo yake.

Ewe Mola! Teremsha salamu na maamkizi Yako bora kabisa kwa Bwana na Kiongozi wetu, Imam Mahdi anayesubiriwa, (as). Utujumuishe sisi na Umma wa Kiislamu katika dua zake takatifu na zinazokubaliwa, uiangazie na kuipamba dunia kwa kudhihiri kwake kwa baraka, kama ulivyoahidi, hakika nyoyo zetu zimejaa yakini juu ya ahadi hiyo isiyobadilika:

وَعَدَ اللَّهُ الَّذِینَ آمَنُوا مِنْکُمْ وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَیَسْتَخْلِفَنَّهُمْ فِی الْأَرْضِ کَمَا اسْتَخْلَفَ الَّذِینَ مِنْ قَبْلِهِمْ وَلَیُمَکِّنَنَّ لَهُمْ دِینَهُمُ الَّذِی ارْتَضَیٰ لَهُمْ وَلَیُبَدِّلَنَّهُمْ مِنْ بَعْدِ خَوْفِهِمْ اَمْنًا

Mwenyezi Mungu amewaahidi wale walio amini miongoni mwenu na wakatenda mema, ya kwamba atawafanya makhalifa katika ardhi kama alivyo wafanya makhalifa wa kabla yao, na kwa yakini atawasimamishia Dini yao aliyo wapendelea, na atawabadilishia amani baada ya khofu yao.

Was-salamu ‘ala jami‘i ikhwanina al-muslimin wa rahmatullahi wa barakatuh.

Dhul-Hijjah 1447 H

Sayyid Mujtaba Husseini Khamenei.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha